Makala
Barazani kwa Ahmed Rajab
Raila ajizuie, vinginevyo….
Ahmed Rajab
Toleo la 288
3 Apr 2013
Raila Odinga

MSIMU wa uchaguzi nchini Kenya ulimalizika rasmi alasiri ya Jumamosi iliyopita, dakika chache kabla ya kutimia saa kumi na moja.

Hapo ndipo Jaji Mkuu, Dakta Willy Mutunga, alipoujulisha ulimwengu uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu uhalali wa Tume ya Uchaguzi kutangaza kuwa Uhuru Kenyatta na mwenza wake, William Ruto, ndiyo washindi wa uchaguzi wa urais uliofanywa Machi 4, 2013.

Mutunga alisema kwamba jopo la majaji sita wa Mahakama Kuu lilikubaliana “kwa kauli moja” kwamba uchaguzi wa urais ulifanywa kwa njia huru na ya haki.

Uamuzi huo ulihitimisha malalamiko yaliyofikishwa mbele ya Mahakama hiyo ya kutaka kumzuia Uhuru asiingie Ikulu na ulikuwa pigo kubwa kwa Raila Odinga aliyekuwa mlalamikaji mkuu mahakamani.

Raila, kiongozi wa Orange Democratic Movement (OD) na wa Muungano wa CORD, ndiye aliyekuwa mshindani mkuu wa Uhuru katika mchuano wa kuuwania urais.

Mlalamikaji mwingine dhidi ya Tume ya Uchaguzi na Uhuru pamoja na Ruto lilikuwa shirika la kiraia la AfriCOG (Kituo cha Afrika cha Utawala Wazi).

Kuna mambo mawili tunayohitaji kuyazingatia kwa makini. Kwanza tusisahau kwamba ni Raila aliyesaidia kufanikisha mageuzi makubwa katika mfumo wa kisheria na wa Mahakama nchini Kenya.

Pili tusisahau kwamba Mahakama yote ya Kenya yanaongozwa na Mutunga akiwa Jaji Mkuu. Huyu ni rafiki mkubwa wa Raila na alikuwa mwenzake aliyeshirikiana naye sana siku za kupigania Katiba mpya na mageuzi ya utawala nchini.

Urafiki wa Raila na Mutunga uliwatia hofu baadhi ya wafuasi wa Uhuru ambao kabla kesi kuanza walimtaka Mutunga ajitoe kwenye kesi hiyo. Wakiamini kwa dhati kwamba atampendelea Raila.

Hadi sasa Mutunga hana doa lolote; hana ila hana waa japokuwa kuna wenye kukirihishwa na hereni anayovaa kwenye sikio lake la kushoto.

Mutunga anasifika na kuheshimiwa kwa uadilifu wake na moyo wake wa kutetea haki. Ni muhimu basi tusisahau kwamba ni yeye aliyeutangaza uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kuyatupilia mbali maombi ya Raila na AfriCOG. Kwa mpigo mmoja uamuzi huo ukamhalalisha Uhuru Kenyatta kuwa rais wanne wa Jamhuri ya Kenya.

Kwa hakika, sitoshangaa ikiwa nitasikia kwamba Raila alikuwa amekwishakata tamaa baada ya mawakili wake na wa AfriCOG kutoa hoja zao.

Ninasema hivi kwa sababu ilikuwa wazi ya kuwa juu ya umahiri wao mawakili hao hawakutoa ushahidi wowote madhubuti uliothibitisha kwamba kura ziliibiwa au kwamba zilifanyiwa kiini macho kiasi cha kuufanya uchaguzi huo uwe na dosari au taksiri kubwa za kuwapelekea watu wautoe maanani.

Walichoweza kufanya mawakili hao ni kuonyesha kwamba Tume ya Uchaguzi ilishindwa hapa na pale kutekeleza hili na lile.

Walionyesha kwamba palifanyika makosa ya kibinadamu na ya mitambo lakini si kwamba kulifanywa njama ya makusudi au mazingaombwe ya kuiba kura au kuzichakachua kura zilizopigwa.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu kama nilivyokwishadokeza ni pigo kwa Raila. Ni pigo kwake kwa sababu sasa, akitaka asitake, lazima ajiinamie na kuutafakari mustakabali wake wa kisiasa. Hii ni mara yake ya tatu kuuwania urais wa Kenya. Mara zote hizo ameshindwa.

Baba yake, Jaramogi Oginga Odinga, aliyekuwa makamu wa rais wa kwanza nchini Kenya, naye pia alijaribu zama zake na alishindwa kuunyakua ufunguo wa Ikulu.

Waliokuwa wakiziangalia karata za uchaguzi wa urais zilivyokuwa zikichezwa walitambua tangu awali kwamba Raila atakwenda kapa. Watu wengi hawakuuamini utabiri huu na ulipokuwa ukiwaambia wanakuangalia kana kwamba wewe ni mwehu.

Ukweli ni kwamba kadiri Raila na Uhuru walivyokuwa wakiukaribia uchaguzi Raila akizidi kuwa dhaifu kwa sababu ya makosa aliyokuwa akiyafanya njiani.

Makosa hayo yaliwasaidia Uhuru na Ruto kuweza kumpiku katika mbinu za uchaguzi kama nilivyoeleza katika makala zilizotangulia katika gazeti hili la Raia Mwema (Mbinu za ushindi za mwana wa Jomo na Changamoto zinazowakabili Uhuru na Ruto ).

Kosa moja alilofanya Raila ni kuzitegemea nchi za Magharibi kuwa zingempatia ushindi katika uchaguzi huo. Sijui ilikuwaje hata akasahau kwamba nchi hizo hazipigi kura katika chaguzi za Kenya.

Kweli zilijaribu kuwashawishi wapiga kura wa Kenya wasiwapigie kura kina Uhuru na Ruto na kwa kufanya hivyo zikitumaini kwamba badala ya kuwapigia kura hao wawili Wakenya watampigia kura Raila na mwenza wake Kalonzo Musyoka.

Sababu kubwa iliyotolewa na nchi hizo ni zile kesi zinazowakabili Uhuru na Ruto mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai mjini Hague.

Bila ya shaka wako waliotekwa na propaganda hiyo. Lakini walikuwa wachache. Wengi wa wananchi wa Kenya waliziona tashwishi hizo kuwa ni njama za madola ya Magharibi za kuingilia kati katika siasa za Kenya na kulishurutisha taifa hilo liwakubali viongozi fulani. Walizifananisha tashwishi hizo na ‘ukoloni mamboleo’.

Ajabu ya mambo ni kwamba hayo mashtaka yanayowakabili akina Uhuru na Ruto huko Hague badala ya kuwaporomoa yalisaidia kuwajenga machoni mwa Wakenya wengi, hasa katika maeneo ya Kati ya Kenya na katika Bonde la Ufa.

Ajabu nyingine ni kwamba hivi sasa mashtaka hayo dhidi ya Uhuru na Ruto yanazidi kuonekana kuwa yasiyo na nguvu.

Kosa la pili la Raila ni kuziamini zile kura za maoni zilizokuwa zikiwababaisha Wakenya na zilizokuwa siku zote zikisema kwamba yeye Raila ndiye atayeibuka mshindi katika uchaguzi wa urais.

Imani hiyo ilimfanya apwaye asijizatiti kama walivyojizatiti mahasimu wake wa Muungano wa Jubilee ukiongozwa na Uhuru.

Wao walifanya juu chini kuwashawishi wafuasi wao waende kujiandikisha kwa wingi katika daftari la wapigaji kura na wajitokeze kwa mkururo kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi.

Hata watoto wa shule wenye umri wa kupiga kura walijiandikisha katika ngome za Uhuru na Ruto.

Kuna na mengine pia yaliyomponza Raila. Kwa mfano, ule unaosemekana kuwa ni udikteta wake uliowasababisha wenzake kadhaa wamuache mkono. Miongoni mwao alikuwa Ruto.

Jingine ni jinsi alivyokuwa akiwapendelea jamaa zake wakiwa pamoja na ndugu zake halisi wakati wa kuwateua wagombea uchaguzi wa ODM kwa nyadhifa mbalimbali.

Wapenzi wa Raila walianza kubabaika baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza Machi 9 kuwa Uhuru na Ruto ndiyo washindi wa uchaguzi wa urais.

Mfano mzuri ulikuwa msimamo wa Muungano wa Ulaya. Kwanza ulitoa ripoti ukisema uchaguzi ulikuwa wa haki lakini baada ya siku mbili, tatu ukabadili msimamo na kuupaka matope uchaguzi huo.

Jambo moja ambalo lazima siku zote tuwe macho nalo ni kwamba takriban asasi zote za kiraia barani Afrika zinafadhiliwa na nchi za Magharibi na zinaendesha shughuli zao kwa kufuata miongozo na ajenda za nchi hizo.

Bila ya shaka si wafadhili wote wenye kasumba ya ukoloni mamboleo na wala si asasi zote za kiraia barani Afrika zenye kasumba hiyo. Zipo za kizalendo zisizokubali kuyumbishwa na ajenda za nchi za Magharibi.

Baadhi ya hizo nchi za Magharibi zimekuwa zikigharimia harakati za baadhi ya asasi za kiraia zilizokuwa na lengo la kuwakaba akina Uhuru na Ruto mpaka ushindi wao uwatokee puani.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya uliotolewa Jumamosi iliyopita umezima jitihada zote hizo. Hivi sasa macho ya wengi yamemgeukia Raila na yanaangalia ataamua kufanya nini baada ya kushindwa kumzuia Uhuru asiingie Ikulu.

Ingawa amesema kwamba anaukubali uamuzi huo hata hivyo inaonyesha kwamba ana dukuduku juu yake kwani matamshi yake mengine yanaonyesha kana kwamba anaamini ya kuwa uamuzi huo haukuwa wa haki. Bado anasema kuwa kuna mzozo ambao lazima utafutiwe njia nyingine za kuusuluhisha.

Kama Raila bado hataki kuziacha siasa anaweza kuendelea kuwa mshabiki wa mageuzi huku akiwa macho kuikosoa serikali ya Uhuru Kenyatta kama itakwenda kombo.

Lakini akiendelea kulalama kila akiamka kwamba amepokonywa urais basi malalamiko yake yanaweza yakachochea fujo. La si hivyo, basi anaweza akajikuta anatwanga maji kwenye kinu huku wenzake wakimtupa mkono na kuikubali hali halisi iliyopo.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Ahmed Rajab
ahmed@ahmedrajab.com

Toa maoni yako