Browse By

Nini kilichotokea kati ya Kolimba na Nyerere? II

WIKI iliyopita katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala hizi, nilieleza katika hali ya kudadisi zaidi ni kwa nini viongozi wengi hawakuwa tayari kumkosoa Mwalimu Julius Nyerere hadharani na kama baadhi walithubutu, basi, walikuwa wachache mno na ukosoaji ulikuwa wa nadra.

Nilieleza kuwa wengi hawakuwa katika ‘mizani’ sawa na Mwalimu kwa kigezo cha uadilifu mbele ya umma na hata wale waadilifu, ilitokea wakiiga njia ya uadilifu wa Mwalimu Nyerere. Lakini pia nilieleza licha ya nguvu hizo za kiuadilifu, Mwalimu alikuwa na ushawishi mkubwa katika mifumo ya kidola nchini.

Mifumo ya kidola ambayo alishiriki kuibuni na kuiridhia, akiwa Mkuu wa Nchi wa kwanza baada ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika na hata Tanzania (baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar).

Nilieleza ni Mwalimu Nyerere ambaye ujasiri wake wa kumkosoa yeyote hadharani, ulivunja mipaka na hadi kumgusa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais aliyekuwa madarakani, Ali Hassan Mwinyi.

Ukosoaji huo pia uliwagusa bila woga, aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela na aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala (CCM), Horace Kolimba. Hawa wote aliwakosoa kupitia kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Makala ilieleza kuwa ni Kolimba pekee kati ya viongozi hao watatu ndiye aliyejitokeza kujibu mapigo dhidi ya Mwalimu kupitia makala maalumu katika magazeti ya chama (CCM), akiwa Katibu Mkuu, huku Mwinyi na Malecela wakibaki kimya.

Nikaeleza, Mwalimu alijua hilo hasa pale alipoulizwa wanahabari na kujibu akitamka maneno sita tu; mwacheni nitajibizana naye hoja kwa hoja. Hata hivyo, katika makala hiyo ya kwanza katika mfululizo wa makala hizi, kulikuwa na makosa.

Nilieleza Kolimba alitamka CCM kupoteza dira akiwa angali Katibu Mkuu wa chama hicho, ukweli ni kwamba alitamka hivyo lakini wakati akiwa tayari ameondoka kwenye nafasi hiyo.

Leo tunaendelea na sehemu hii ya pili ya mfululizo wa makala hizi. Katika sehemu hii ya pili, naanza kuchambua hoja za Kolimba katika kujibu mapigo dhidi ya Mwalimu Nyerere.

Kolimba ambaye kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala hizi, tayari alikuwa na nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Inawezekana ukosoaji wa Mwalimu dhidi yake aliutafsiri kama kikwazo na kwamba Mwalimu ameingilia nia yake hiyo (lugha ya siku hizi kumchafua-sio kumkosoa).

Inadaiwa kuwa Kolimba kupitia kwa mwandishi aliyetambulishwa kwa jina la Alex Kowe, aliandika makala katika gazeti la Uhuru, Novemba 8, 1994, takriban miezi 10 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 1995.

Miongoni mwa hoja zake katika makala husika ni malalamiko dhidi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Anamlalamikia Nyerere kwa kile anachokieleza kuwa ni hatua yake ya kumlazimisha Rais Ali Hassan Mwinyi, asipokee ushauri wake (Kolimba).

Ni Nyerere pekee angeweza kufafanua hili ingawa pia inawezekana alimuonya Mwinyi kutopokea ushauri wa Kolimba pengine baada ya kubaini ni aina ya kiongozi asiyeaminika kwa kiwango cha kuridhisha katika baadhi ya masuala ya kiuongozi.

Ni kutokana na maelezo ya Nyerere kwa Mwinyi kwamba ushauri wa Kolimba ni wa shaka, Kolimba mwenyewe anapinga hilo akisema haikuwa sahihi kwa sababu anaamini si wakati wote angekuwa na ushauri mbaya au ushauri wenye nia mbaya kwa Rais Mwinyi.

Ni katika mazingira hayo ya kumuonya Mzee Ali Hassan Mwnyi kutoamini moja kwa moja ushauri wa Kolimba, kuna maelezo pia yanayodai kwamba Nyerere alikuwa akimwona Rais Mwinyi kuwa ni kiongozi aliyezongwa na udhaifu wa kiuongozi.

Udhaifu aliouona Nyerere kwa Mzee Mwinyi unadaiwa ni kuhusu namna ya kuchuja (kupima) ushauri kutoka kwa viongozi wengine wanaomsaidia na hapa, izingatiwe kuwa, ushauri mbovu ni msingi wa uamuzi mbovu.

Kwa hiyo, Kolimba kupitia makala hiyo ambayo inadaiwa kuandikwa naye ingawa ilipewa jina (by-line) la Alex Kowe, anapingana na Nyerere kuhusu hoja ya udhaifu wa Mwinyi kiuongozi. Katika kupinga, Kolimba anadai kwamba udhaifu wa Mwinyi si kushindwa kuchuja (kupima) ushauri bali ni uungwana wake kupita kiasi.

Anasema Mwinyi ni muungwana kupita kiasi. Kwa  mujibu wa Kolimba, msingi wa uungwana huo wa Mwinyi uliovuka mipaka ni mwelekeo wake wa kuchelea kumuudhi (kutompinga) Baba wa Taifa na hivyo kumpa mwanya wa kumyumbisha.

Kwa lugha nyingine, wakati Nyerere anaamini Mzee Mwinyi ni dhaifu katika baadhi ya masuala ya kiuongozi na hasa kupima ushauri anaopewa na wasaidizi wake, Kolimba aliamini huo si udhaifu kwa tafsiri halisi ya udhaifu, bali ni uungwana uliopita kiasi ambao Nyerere ‘aliutumia’ kumyumbisha Mwinyi kiuongozi.

Kolimba anamgeukia Nyerere akijibu mapigo kutoka kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania dhidi yao (Kolimba na wenzake Mwinyi, Malecela) akimwelezea (Nyerere) kuwa ni mtu ambaye haambiliki na ni king’ang’anizi.

Katika mashambulizi yake kwa Nyerere ambaye tayari katika makala iliyopita tuliona alifuatwa na waandishi wa habari na wakamuuliza kuhusu mashambulizi dhidi yake kutoka kwa Kolimba naye akawajibu; mwacheni aendelee nitajibishana naye hoja kwa hoja, Kolimba anasema Nyerere akishikilia jambo lake huwa hashauriki kwa urahisi na wala hashawishiki.

Katika sentensi fupi akimwelezea Nyerere, Kolimba kupitia makala anayodaiwa kuiandika na kubandika jina la Alex Kowe, anamtafsiri akisema kwake (Nyerere); “msimamo kwanza na maslahi baadaye.”

Kolimba anatetea tafsiri yake hiyo dhidi ya Nyerere (msimamo kwanza na maslahi baadaye) akiorodhesha mambo ambayo anaamini Nyerere aliyasimamia kwa kutanguliza msimamo badala ya maslahi ya nchi na hivyo, hayakuwa na mafanikio mazuri kwa nchi.

Mambo hayo ambayo Kolimba anaamini yalitekelezwa kwa msimamo usioridhia ushauri ni kwanza; Azimio la Arusha. Pili, operesheni vijiji. Tatu, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokuwa ikiundwa na nchi tatu- Tanzania, Kenya na Uganda (mwaka 1977).

Nne, mapambano yake (Nyerere) ya muda mrefu dhidi ya sera za Shirika la Fedha duniani (IMF), kwa wakati huo Mwalimu akikerwa mno na masharti ya shirika hilo kwa nchi masikini akifikia hatua kutamka IMF si Wizara ya Fedha ya Dunia.

Kolimba katika makala hiyo anayodaiwa kuiandika yeye, anamkabili Mwalimu akisema mambo hayo manne ni mifano na vielelezo vya misimamo mikali ya kisiasa ya Mwalimu Nyerere, ambayo haikutanguliza mbele maslahi ya taifa na watu wake. Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hizi kuhusu nini kilichotokea kati ya Kolimba na Mwalimu Nyerere?

Wiki ijayo tutachambua namna wakati fulani Kolimba alipofurahia ‘kusita’ kwa Mzee Mwinyi kukidhi haja za shinikizo la Mwalimu Nyerere, kutaka yeye (Kolimba) na Malecela waondolewe madarakani. Tutaangalia je, Kolimba alichukuliaje uamuzi huo wa Mwinyi ambao hata hivyo, baadaye waliondolewa madarakani.

Kwake yeye Kolimba, kitendo cha Rais Mwinyi kukataa shinikizo la Mwalimu Nyerere kutaka Malecela na yeye waondolewe madarakani (jambo kuchelewa kutekeleza shinikizo hilo) ni kitendo cha ujasiri na wala si kielelezo cha udhaifu kama ambavyo Nyerere angetaka Watanzania waamini.

Inaendelea

8 thoughts on “Nini kilichotokea kati ya Kolimba na Nyerere? II”

 1. Msomaji Raia Mwema says:

  Bwana Dilunga;

  Umefanya vizuri kusahihisha historia.

  Ombi: Ingekua vizuri kama makala zako zingekua zinajitegemea. Hii ya leo ni nusu ya ile iliypita na habari mpya ndio nusu nyingine. Pamoja na kua ni lazima kutoa muhtasari wa habari iliyopita ili kua na mfululizo mzuri wa makala, muhtasari wako leo umekua mrefu sana, na sidhani kama bado tutauita muhtasari bila kupoteza maana ya hili neno.

  Binafsi ningependa sana kujua kiini cha tofauti kati ya Mwalimu na Kolimba. Hizi ni simulizi za maana kwetu Watanzania kuelewa historia yetu kupitia tabia na maamuzi ya viongozi wetu

  Ahsante wa kutuelimisha.

  Msomaji Raia Mwema.

   

 2. Uncle D says:

  Dilunga na Magig tunashukuru kwa kuchokonoa vitu ambavyo miongo michache iliyopita kufanya hivo ilikuwa ni uhaini.

 3. Msomaji wetu says:

  Naungana na msomaji wa raia mwema aliyetangulia kutoa maoni kukushukuru kwa kurejea historia za viongozi wetu waliotangulia hasa katika mada hii. Tunasubiri kwa hamu kuona muendelezo wa mada hii.

 4. WABHUKHABHA says:

  NYERERE ALIKUWA MTU WA KAWAIDA TU ALIYEAMINI ALICHOKUWA  AKIAMINI.ALISEMA ALICHOKUWA ANAAMINI. ROHO YAKE ILIKUWA SAAFI NA NDIO MAANA TUNAMKUMBUKA.

 5. JS says:

  Ni Makala ya Kuvutia!!

  Hii huenda ikawa makala ya kuvutia sana. Kama mfuatiliaji wa makala au maandishi yeyote ya kisiasa nchini naona hii makala inaweza kuwa nzuri.

  Hata hivyo, nitoe maoni yangu ya mwanzo. Katika sehemu hii ya pili na makala yako umegusia suala la Benki ya Dunia na Taasisi yake ya IMF.

  Niseme kwa kifupi kuwa Mzee Mtei alipotoa kitabu chake cha wasifu wake " na mle ndani kueleza kwa kirefu kwa nini alitofautiana na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere; hasa kuhusu maelekezo ya Benki ya Dunia na taasisi yake ya IMF, nabaini kuwa Baba wa Taifa ilikuwa sahihi.

  Mara baada ya Mzee Mtei kutoa kitabu chake hicho na baada ya kukisoma nilikutana na mwananchi mmoja wa Uganda, ambaye kwa miaka mingi alifanyakazi Benki ya Dunia, Washington , na IMF. Bwana yule anaitwa Dkt Okello. Yeye nilipomsimulia tofauti ya Nyerere na Mzee Mtee kuhusu Benki ya Dunia alisema moja kwa moja kuwa Nyerere u sahihi na kusema kuwa Mtei kudai kuwa masharti ya Benki ya Dunia ni dawa ya kila kitu ni mawazo potofu.

  Ushauri wangu kwako, jaribu sana katika kuendeleza makala hii nzuri, jaribu kupata taarifa sahihi na kuzifanyia uchambuzi wa kina kabla ya kufikia hitimisho. Usiwe kama Majidi Mjeng'w ambaye huuaza na makala nzuri lakini makala huushia shagala ba galaK_ keo ya nchi!Q!

 6. Msomaji Raia Mwema_Nyamburi says:

  Ni Makala Nzuri!!

  Hata hivyo, naomba unapoendeleza makala hii, na hasa, kwa kuwa umemtaja Baba wa Taifa dhidi ya msimamo wake na IMF basi nakushauri usome kile kitabu cha Wasifu wa Edwin Mtei. Ndani ya kitabu kile anataja kwa nini alitofautiana na Nyerere!

  Binafsi nilikisoma na kubaini Nyerere alikuwa sahihi katika msimamo wake wa kutokububali masharti ya IMF na Benki ya Dunia. Yeye Mtei aliyekubali Masharti ya IMF na Benki ya Dunia ndiyo wamefikisha elimu yetu hapa tulipo. Walitulazimisha kufuata mambo ya Ulaya ambayo si sahihi kwa nchi maskini kama Tanzania.

 7. john says:

  Hizi ndizo makala ambazo tunahitaji kusoma. Lakini ufanye homework yako sawa sawa kabla ya kuandika makala . Na, usipende kuileta katika vipande vifupi, vifupi saana

 8. Kirebro says:

  Bwana Dilunga!!

  Kama itawezekana wasomaji wengi wangependa kufahamu vile vile  ni nini hasa Kambona na Nyerere hawakuelewana. Kambona aliikimbia nchi na kuzeekea Uingereza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *