Makala
Kikwete anazima moto kwa petroli
Msomaji Raia
Toleo la 213
23 Nov 2011

NIANZE makala hii kwa kumbukumbu maalumu. Siku moja nilibahatika kupata heshima ya kukaa meza jirani na alipokuwa amekaa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Tulikuwa tunakula chakula cha mchana na yeye alikaa na waheshimiwa wengine wakizungumza masuala yanayohusu nchi na maisha kwa ujumla.

Mkapa ni mmoja wa watu ninaowathamini sana kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja na kuzisimamia. Kwa hiyo, siku hiyo nilikula chakula changu taratibu sana huku nikitega masikio ili kusikiliza mazungumzo yasiyonihusu.

Kipindi hicho, Rais Jakaya Kikwete alikuwa amehutubia viongozi wa dini na kufafanua suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi hapa nchini. Katika hotuba ile, Rais Kikwete alidai kuwa hoja ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi ilianzishwa na Mkristo, Augustine Mrema, ikaendelezwa na Mkristo Thomas Ngawaiya. Akaendelea kusema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM iliyotumika mwaka 2005 na kuingiza ahadi ya kuanzisha mahakama ya kadhi, iliandaliwa chini ya usimamizi wa viongozi wa CCM walio wakristo yaani Benjamin Mkapa na Philip Mangula. Akajitetea katika hotuba ile kuwa yeye alikabidhiwa ilani hiyo uwanja wa Jangwani na kwenda kuinadi kwa Watanzania. Kimsingi, Kikwete alikuwa anajaribu kujiosha lawama mbele ya wakristo kuwa yeye hahusiki na suala hilo bali ni wao walioasisi hoja hiyo. Historia imejirudia pale alipowageuka waislam na kusema Katiba hairuhusu wakati ni CCM iliyoahidi ndani ya ilani yake. Tabia hii naiita ya kuzima moto kwa kutumia mafuta ya petroli.

Kutokana na hotuba hiyo ya Kikwete nilimsikia Rais mstaafu Mkapa akicheka kicheko cha kejeli na kusema “nadhani hajaelewa maana ya Presidency”, kisha akaongeza, “ukiwa Rais unarithi yote; hakuna nafasi ya kulaumu wengine”. Baada ya michango ya wenzake pale mezani, Rais Mkapa alihoji “Kwani yeye ni robot?” Nadhani alilenga kusema Rais ana mamlaka na utashi katika kutekeleza majukumu yake na kwa hiyo anapaswa atumie akili pia, siyo kutekeleza kama mashine.

Masengenyo ya Rais Mkapa kwa utawala wa awamu ya nne yamenifanya kutafakari na kutathmini sana mtindo wa utawala huu tulio nao. Kila kukicha utawala huu unafanya uamuzi unaozua maswali mengi kuliko majibu. Matokeo ya mtindo na mfumo wa uongozi na utawala huu, taifa linajikuta likitengeneza migogoro mingi kuliko uwezo wake wa kuitatua.

Fikiria kwa makini: CCM iliingia kwenye uchaguzi bila ahadi ya kuleta Katiba mpya. Ghafla ikatoka usingizini baada ya matokeo mabaya ya uchaguzi na kuahidi kuleta Katiba mpya. Huku tukiwa bado tumeduwaa na ahadi hii ya ghafla, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Katiba na Sheria, wakabeza ahadi za Serikali yao kuwa Katiba mpya haihitajiki.

Rais Kikwete bila kujali mgongano huo wa watendaji wake, akaja na maelezo yaliyoonyesha kuwa lengo ni kuboresha Katiba iliyopo. Baada ya kelele za wapinzani, akabadili na kusema lengo ni Katiba mpya lakini akamtuma Mwanasheria Mkuu kwenda bungeni na muswada wa kurekebisha Katiba. Hata wabunge bubu walipolalamika, akauondoa muswada bungeni ‘kiaina’ na kuahidi kuleta muswada mpya.

Muswada uliporejeshwa bungeni wiki iliyopita ukaja kwa sehemu kubwa ukiwa ni mpya lakini kwa shinikizo kuwa unasomwa kwa mara ya pili na si ya kwanza. Kulikoni tena muswada mpya unasomwa kwa mara ya pili? Wapinzani wakasusa; wabunge wa utawala wakajadili kususa badala ya muswada mpya. Kura za mkumbo zikapigwa na muswada ukapita kwa kishindo cha kushinda bila kushinda. Kana kwamba hiyo haitoshi, Rais akahutubia wazee wa CCM jijini Dar es Salaam na kusisitiza atausaini muswada ili uwe sheria.

Si mara ya kwanza Kikwete kusaini muswada wenye makosa. Alisaini muswada wa gharama za uchaguzi kwa mbwembwe akalazimika ‘kulamba’ wino wake kabla haujakauka kwa sababu ya makosa yaliyogunduliwa na wapinzani ndani ya muswada huo. Kabla ya kuwa Rais, aliwahi kusaini mikataba inayolitesa taifa mpaka leo. Kwa hiyo ni mjuzi wa kusaini nyaraka zenye makosa na mara zote wasaidizi wake wamelaumika kana kwamba yeye hana utashi binafsi wa kutambua makosa anayosaini.

Kwa hili la Muswada wa Marekebisho ya Katiba badala ya muswada wa kutengeneza Katiba mpya, Kikwete amevurunda zaidi. Hatua yake ya kupuuza kelele za baadhi ya wanaharakati na wapinzani, zimekwenda sambamba na jeuri ya kudhoofisha mihimili mingine na kwa hiyo, kuasisi “urais wa kifalme” (Imperial Presidency). Kitendo cha Spika, Anne Makinda kuburuza wapinzani hakikuwa uamuzi wake bali madai ya Rais Kikwete kuwa yeye ni “mkuu wa nchi” na hii ina maana kuwa “mkuu wa nchi” yuko juu ya mihimili yote na kimsingi, yuko juu ya sheria.

Hatua ya Spika kuburuza wabunge, na madai ya Kikwete kuwa ni mkuu wa nchi si tu yaliwakatisha tamaa wapinzani, bali pia yaliwafunga midomo na mikono wabunge wachache ndani ya CCM waliojijengea tabia ya kusema ukweli. Hao nao walilazimika ama kuomba radhi kama walitaka kuchangia muswada kwa njia ya kuukosoa au waliamua kukaa kimya na kujiunga na wanaozomea na kumjadili Tundu Lissu. Hatimaye muswada ulipita kama Rais alivyotaka na kulifanya Bunge kuwa sehemu ya Rais, kama Rais alivyo sehemu ya Bunge.

Mhimili wa Mahakama hatuwezi kuusemea sana hapa, lakini itoshe tu kudokeza kuwa, sauti za majaji wastaafu, sauti ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na baadhi ya maprofesa wa sheria, zinaashiria kuwa kuna kasoro kubwa katika muswada uliopitishwa kwa shinikizo la Rais anayetamani udikteta. Kwa kuwa sasa ni wazi kuwa Rais wa sasa ni kila kitu – yaani ni Bunge, Mahakama na mkuu wa nchi, basi hata Katiba itakayoundwa chini ya muswada huu, inaweza kuwa mbaya kuliko hata hii ya sasa. Kwa nini?

Kwanza, tunadai tunatengeneza Katiba mpya wakati tunakarabati iliyopo. Pili, tunadai tunafuata mtindo wa Kenya wakati si kweli kwa sababu wajumbe wa tume ya Kenya waliwasilisha maomba ya kuwa wajumbe na kuchujwa kisha Rais akathibitisha uteuzi tu.

Tatu, ni wazi Rais tayari ana majina ya wajumbe wa tume na wengine tayari wametuambia kuwa amewaahidi. Nne, hadidu za rejea anazo yeye (ingawa angalau kuna mabadiliko yamefanyika) lakini pia hata maoni anayotaka yeye yatapelekwa kwa wananchi ili yakubaliwe.

Tano, tayari muswada unazuia maeneo fulani kuwa yasiguswe bali yaboreshwe. Sita, vyombo vya dola vimeagizwa kuwakamata wanaopinga muswada huu. Hii ina maana vyombo vya dola vijifunze siasa kwanza ili kujua nani anachangia kwa kupinga na nani anachangia kwa kuunga mkono. Saba, Rais Kikwete amekutana na wabunge wote wa CCM na kuwaagiza waende majimboni kuwahamasisha wananchi ili waunge mkono muswada huu. Kwa maneno mengine, haitarajiwi kwa mwana CCM safi kupingana na muswada huu.

Naweza kuonekana mchochezi, lakini yawezekana kuwa Rais Kikwete ameishaandika Katiba mpya, anayo Ikulu na anasubiri mwaka 2014 aiweke hadharani. Haiingii akilini kwa Rais anayependa ustawi wa taifa lake akatae maoni ya watu fulani na kujifanya kuwa ni yeye anayejua Watanzania wanataka nini.  Na ikiwa huu ndiyo mtindo unaotumika kwa mchakato huu wa Katiba, si ajabu kuwa hata fikra zilizozagaa miongoni mwa Watanzania kuwa chaguzi zinazofanyika huwa ni kiini macho bali kura huwa zimeishapigwa na matokeo kupangwa kwa kadri ya mapenzi ya watawala. Nani atasita kuamini kuwa hata kura ya maoni inayotajwa katika muswada huu itahakikishwa kuwa matokeo yake yanakuwa kwa kadri ya mapenzi ya watawala?

Dalili za kuthibitisha ukweli huu ni hizi ambazo Rais na chama chake wanalazimisha mchakato uende wanavyotaka wao.

Nimetangulia kusema kuwa Rais Kikwete anazima moto kwa kutumia mafuta ya petroli. Kuteka mchakato wa kutengeneza Katiba mpya kwa njia ya vitisho, vijembe, ushabiki wa kiitikadi, kuhutubia wazee badala ya vijana na kutumia ujasiri wa kuazima mbele ya kadamnasi, kunainyima uhalali Katiba hiyo kabla haijazaliwa.

Kitakachotokea ni kuzaliwa kwa Katiba inayoitwa mpya lakini madai ya kudai Katiba yatabakia. Kama ambavyo CCM kimebakia kuwa chama cha viongozi, hata Katiba itakayozaliwa na muswada uliokiuka taratibu, itakuwa Katiba ya watawala wetu. Ni Katiba inayoshughulikia kuwapata viongozi na kuwakikishia starehe wakati wote wa kututawala. Tukifika hapo, hata mitaro ya maji taka haitatosha kuwasitiri watawala wetu pale puto litakaporipuka.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Msomaji Raia
msomajiraia@yahoo.co.uk

Maoni ya Wasomaji

Ni hatari

MIMI KURA YANGU KWA AJILI YA HUU MUSWADA NINAYO HAPA NI "HAPANA" MUSWADA HUU WA KATIBA HAUFAI, 

Toa maoni yako