Makala
KUTEKWA KWA KIBANDA
Kibanda ni Nani? Mwanahabari, Mnyakyusa, na Mkristo
Msomaji Raia
Toleo la 285
13 Mar 2013
Absalom  Kibanda akiwa hospitalini alipotembelewa na Rais Kikwete

NIANZE kwa kuomboleza msiba wa jicho moja la Absalom Kibanda. Jicho hilo lilijeruhiwa na watu wabaya usiku alipotekwa na kupigwa na watu hao.

Tumejulishwa kuwa madaktari wanne walijitahidi sana kuokoa jicho hilo lakini wameshindwa na kuthibitisha kuwa jicho hilo limekufa rasmi. Kiungo kimoja na cha muhimu sana cha mwili wa Kibanda kimetoweka.

Hatukuhudhuria mazishi ya kiungo hicho lakini inatosha tukiamini kuwa kiungo hicho hatunacho tena. Kimetoweshwa. Kimetoweshwa na watu waoga. Mola alaze mahali pema peponi, jicho la ndugu yetu Absalom Kibanda. Amina.

Kwa kuwa sasa ni wazi taifa letu linaangamizwa na ombwe la utawala, ni sahihi nikisema kuwa kutekwa, kupigwa na kuumizwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Bwana Absalom Kibanda, si jambo la bahati mbaya. Lina dalili za kupangwa kwa makini na watu wenye akili za uharibifu.

Nasema hivyo kwa sababu, Absalom Kibanda ana vigezo vyote vitatu ambavyo vimekuwa vinausumbua sana mfumo wetu. Na sifa moja ya watu dhaifu huwa ni “kuwaondoa” (eliminate) watu wanaoonekana wana ujasiri wa kuwakosoa. Vigezo vitatu alivyo navyo Kibanda kiasi cha kuwavutia majasusi waliomteka na kumuumiza ni kwa kuwa ni mwanahabari, Mnyakyusa na ni mkristo.

Waandishi wa habari ni moja ya makundi ambayo kwa kawaida huwindwa na tawala dhaifu popote duniani. Tawala hizo huanza kwa kuweka sheria kandamizi na kali kudhibiti uhuru wa habari. Hilo Iinaposhindikana hutafuta mbinu ya kuwanunua waendane na utawala dhaifu. Hilo likishindikana ndipo huanza kuwaondoa mmoja baada ya mwingine au kuwapa ulemavu utakaozuia wao kuendelea na kazi zao kwa ufanisi.

Mazingira yetu yanaashiria ya kuwa tumeishapitia hatua hizo kwanza kwa kuendekeza sheria kandamizi zinazokandamiza uhuru wa habari. Katika miaka saba iliyopita tumeshuhudia kufungiwa kwa magazeti kadha wa kadha kama Mwanahalisi (mara mbili), Kulikoni na hata mitandao ya kijamii.

Tumeshuhudia waandishi wa habari wakiundiwa kesi za ajabu na kupelekwa polisi na mahakamani. Tumeshuhudia waandishi wa habari wakipigwa, kunyang’anywa vitendea kazi na kuuawa na polisi.

Tumeshuhudia mara kadhaa waandishi wakishambuliwa na kuingiliwa katika ofisi zao wakiwa kazini. Katika matukio hayo yote, hakuna mtu aliyekamatwa, kushitakiwa na hatimaye kutiwa hatiani. Badala yake tumeona machozi ya mamba yakitiririka katika mashavu ya watawala kuomboleza majanga hayo yanayowapata wana habari.

Tumeshuhudia misusuru ya magari wakienda hospitalini kuwaona majeruhi na kutoa ahadi za kusaidia matibabu na zile za kuhakikisha wanakamata waliohusika. Wenye hekima wanaamini kuwa serikali yenye mkono mrefu haiwezi kushindwa kukamata mhalifu, ikishindwa, kuna jambo. Imani hii imejengeka mioyoni mwa Watanzania na haiwezi kufutika kwa ahadi hewa.

Absalom  Kibanda Kibanda ni Mnyakyusa anayetoka Mbeya. Katika hali inayoshangaza watu wengi, Mbeya ni Mkoa ambako wanatoka watu wengi waliokumbwa na masaibu ya kutekwa, kupewa sumu, na kuuawa katika mazingira tata. Hata kama baadhi ya matukio hayana uthibitisho, lakini watu wengi wamefanywa kuamini tuhuma chanzo cha masaibu yaliyowapata watu watokao Mbeya na kutishia maslahi ya watawala.

Tumepata kusikia habari za Mbunge wa Kyela na Waziri wa sasa wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe ambaye inadaiwa alipewa sumu inayoendelea kuitafuna ngozi yake. Baada ya dana dana za polisi na kigugumizi cha kusema wazi chanzo cha ugonjwa wa Dk. Mwakyembe, serikali iliona ni vema apozwe kwa kupewa cheo kinachomnyima uhuru wa kuvunja kiapo cha uwajibikaji wa pamoja. Kwa sababu anazozijua, amethamini cheo kuliko uhai wake. Laiti angefuta tuhuma alizozimwaga hadharani kabla hajapewa vyeo hivi!

Tumewahi kusikia tetesi zinazotatanisha kuhusu kuugua kwa Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Rungwe na Waziri asiye na Wizara Maalumu. Inashangaza kwa nini atafutwe kuangamizwa na watu hawa kama tetesi hizo zina ukweli wowote. Lakini kimsingi, tawala dhaifu na dhalimu huwaogopa sana watu wenye uwezo kiakili. Profesa Mwandosya anatoka Mbeya pia na ni yeye, serikali na Mungu wetu wanaojua nini chanzo cha ugonjwa wake.

Tulishuhudia kutekwa, kuteswa na hatimaye kutupwa porini kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka. Yeye pia anatoka Mbeya sawasawa tu na Kibanda pamoja na wengine niliowataja. Mpaka sasa amekaa kimya lakini kuna mawili yanayohitaji ufafanuzi kutoka serikalini.

Kwanza, kwa nini ililifungia gazeti la Mwanahalisi wakati lilikuwa linaisaidia serikali kujua ni kina nani waliohusika kumteka Dk. Ulimboka. Katika hali ya kawaida tungedhani baada ya watawala kusema serikali haihusiki na utekaji huo, basi serikali ingefanya kazi na Mwanahalisi katika kuwatafuta waliohusika maana Mwanahalisi lilionekana kujua ni kina nani.

Pili, kwa nini serikali haitoi taarifa juu ya uchunguzi ilioufanya kuhusiana na sakata hilo? Kukosekana kwa maelezo ya masuala haya mawili, kunauachia umma njia moja tu ya kulielewa suala hili- nayo ni kuwa, mtekaji anajulikana, mtekaji analindwa, na alitumwa kwa sababhu ambazo umma hauwezi kuzijua.

Ndipo likaja la David Mwangosi kuuawa mikononi mwa polisi. Suala hili liko mahakamani lakini itoshe kusema tu ya kuwa Mwangosi pia anatoka Mbeya na alikuwa ni mwandishi wa habari.

Sifa nyingine ya tawala dhaifu huwa ni kuua watu kwa mashinikizo ya imani za kishirikina na ndiyo maana baada ya utawala wa Idd Amin kuanguka, vilikutwa vichwa vya watu katika majokofu ya Ikulu na hata kutunza baadhi ya vifaa vya marehemu kwa sababu zisizojulikana.

Aidha, ilibainika kuwa utawala huo ulikuwa na kiu ya pekee ya kuua watu wa eneo fulani kwa sababu ambazo hazikuwa zikitajwa hadharani na wauaji hao. Baadhi ya wahanga wa tawala dhalimu na dhaifu huwa wanakatwa baadhi ya viungo vyao na wao kushiriki katika mazishi ya viungo vyao wao wenyewe! Nachelea kusema kuwa tunaelekea huko kwa sababu kiu ya viungo vya miili ya wana habari ni kubwa mno kwa sasa.

Absalom Kibanda ni Mkristo sawa tu na wengine niliowataja hapo juu. Siku za karibuni tumeshuhudia makanisa yakichomwa moto (takribani 54 mpaka sasa nchini kote). Tumeshuhudia wakristo wakifunguliwa kesi na polisi kwa kosa la kuchinja vitoweo vyao (takribani kesi 16 nchini kote).

Tumeshuhudia wachungaji na makasisi watatu wakiuawa (Mto wa Mbu, Geita na Zanzibar). Tumeshuhudia makasisi na maaskofu wakishambuliwa kwa risasi na silaha nyinginezo (Zanzibar, DSM na Mwanza). Tumeshuhudia serikali kupitia mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wakitoa amri za kidini kana kwamba wamegeuka makadhi. Tumeshuhudia mzaha wa kuyaambia makundi yanayohasimiana kidini kuwa yakae yamalize tofauti zao.

Tumeshuhudia vipeperushi na kanda za kuhamasisha mauaji ya viongozi wa dini huku serikali ikiwaambia viongozi wa dini wajilinde. Tawala dhaifu na dhalimu huwahofia sana viongozi wa dini na dini yao. Kwa hiyo yaweza kuwa hatari zaidi kuwa mwandishi wa habari na hapo hapo ukawa katika dini inayohofiwa.

Kwa kuwa haya yaliyotajwa hapo juu hayajapatiwa majibu, yametoa mwanya kuruhusu bongo mbalimbali kufikiria zinavyotaka. Mathalani, wapo waliosikika wakisema kuwa Kibanda amepata adhabu kwa sababu ama yeye, au mmoja wa waandishi wake, aliandika taarifa inayotuhumu dini fulani kuwa imeweka kambi ya kigaidi huko Ukerewe-Mwanza.

Kwamba, hata baada ya kuambiwa aombe radhi alikataa. Kwa nini basi kama hilo lilitokea, watu wasiamini kuwa kundi lililomtaka aombe radhi linahusika na utekaji wake?

Watu wengi wasomi kwa watu wa kawaida wanaanza kuona kwamba taifa letu limekumbwa na udini. Kwa hiyo ni sahihi pia kufikiri kuwa, hata kama haipendezi, kuwa suala la dini ya Kibanda lisipuuzwe. Hii hoja ni nyepesi kama dola yetu ilivyo nyepesi na inavyopenda majibu mepesi kwa maswali magumu.

Nimalize kwa kumtakia uponyaji wa haraka Absalom Kibanda. Jicho lake lililoharibiwa limesababisha hata vipofu wapate kuona kinachoendelea katika taifa letu. Damu yake iliyomwagika bila hatia itaharakisha harakati za kulipatia taifa letu dola iliyo imara na thabiti ya kulinda uhai wa watu wake. 

Jicho la mwandishi ni jicho la jamii. Kumtia upofu mwandishi ni kuitia jamii upofu. Ni watawala vipofu tu wanaotamani kufanya kazi na waandishi vipofu.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Msomaji Raia
msomajiraia@yahoo.co.uk

Toa maoni yako