Habari
Kashfa ya vyeo Polisi
Mwandishi Wetu
Toleo la 293
8 May 2013
Msemaji wa Jeshila Polisi, Advera Senso
  • Udini, ukabila, rushwa vyatumika

WAKATI Jeshi la Polisi likipitishiwa na Bunge bajeti ya takriban Sh. bilioni 364.2 kwa mwaka wa fedha 2013/2014, uongozi wa juu wa jeshi hilo unatuhumiwa kuwapandisha vyeo baadhi ya maofisa wake kwa upendeleo, hatua ambayo imezua malalamiko miongoni mwa maofisa wengine ndani ya jeshi hilo.

Kitendo hicho kinatajwa kuwa kinyume cha kanuni (police general order) za uendeshaji wa jeshi kama zinavyoainishwa na Tume ya Utumishi ya Jeshi la Polisi na Magereza.

Habari zilizopatikana kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam, zinadai kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu katika upandishaji vyeo baadhi ya maofisa polisi, kwa vigezo vya urafiki, undugu, udini, ukabila na hata rushwa.

“Utaratibu wa upandishwaji wa vyeo ndani ya Jeshi la Polisi, unapaswa kuzingatia vigezo vinavyoelekezwa ndani ya PGO (Police General Order). Kwanza ni lazima polisi husika awe ametimiza miaka mitatu tangu apande cheo kimoja, lazima mwenendo wa tabia yake uwe mzuri na lakini pia uwe umependekezwa na mkubwa wako wa kazi kupandishwa cheo,” kinasema chanzo kimoja cha habari hizi kikitoa mfano wa upandishaji wa vyeo uliofanywa na Jeshi hilo Aprili 3, mwaka huu.

Katika upandishaji huo wa vyeo wa hivi karibuni, uliowahusu maofisa wa polisi wenye vyeo vya Wakaguzi Wasaidizi kwenda Wakaguzi, Warakibu Wasaidizi wa Polisi (ASP) kwenda Warakibu wa Polisi (SP) na Warakibu wa Polisi kuwa Warakibu Waandamizi, inaelezwa kwamba walipandishwa wa karibuni na kuachwa wa zamani hali inayokiuka kigezo cha utumishi wa muda mrefu.

Kwa mfano, maofisa wanaodaiwa kupandishwa vyeo ni wenye namba PF15834, PF15877 na PF15914, huku wakiachwa wenye namba PF 15164, PF15165, PF15166, PF15167, PF15171 na PF 15174, ambao kwa namba zao hizo wanabainika kuwapo katika utumishi wa muda mrefu.

Aidha, inadaiwa katika upendeleo huo, mmoja wa askari polisi makao makuu amepandishwa vyeo vitatu kwa mpigo, kutoka Mrakibu Msaidizi wa Polisi hadi kuwa Mrakibu wa Polisi Mwandamizi na hivyo kuwa na cheo sawa na askari polisi wenye namba PF13953, PF13958 na PF14085.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari vya kuaminika, mwaka 2011 kundi la maofisa 250 walipandishwa vyeo kwa mpigo na mwaka huu wamechomolewa miongoni mwa hao maofisa 161 tu na kupandishwa vyeo, huku wengine kuachwa wakati wote walikuwa hawajatimiza miaka mitatu kama inavyoelekezwa ndani ya PGO tangu wapandishwe mwaka 2011.

Miongoni mwa hao waliopandishwa wamedaiwa kupangiwa vituo vya Tanga, Arusha na Kigoma wakiwa ni wakuu wa kitengo cha usalama barabarani (RTO’s).

Juhudi za kumpata Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema ili kuzungumzia kadhia hii hazikufanikiwa, lakini Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, anasema utaratibu wa kupandisha vyeo huzingatia taratibu, kanuni, sheria na miongozo ya Jeshi la Polisi, na si suala la mtu mmoja kulala na kuamka na kupandisha vyeo watu.

Kwa mujibu wa Senso, ambaye naye amepandishwa vyeo vitatu kwa mpigo, kutoka Mrakibu Msaidizi wa Polisi hadi Mrakibu Mwandamizi, uadilifu na uchapakazi ni moja ya mambo yanayozingatiwa katika taratibu na miongozo hiyo ya upandishaji wa vyeo jeshini.

Anasisitiza upandishaji wa vyeo haufanywi na mtu binafsi, bali Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi na Magereza nchini. 

Lakini vyanzo vingine kadhaa vya habari hizi vinaeleza kwamba baadhi ya maofisa wa polisi walioko makao makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam, wamekuwa wakipandishwa vyeo bila hata kufuata vigezo vinavyotakiwa kuhusu kupandisha madaraja kwa maofisa wa polisi, vikieleza kwamba “inategemea siku hiyo mkubwa ameamkaje,” suala ambalo linadaiwa kuibua malalamiko kwa baadhi ya askari polisi hao.

“IGP Saidi Mwema anastaafu kwa mujibu wa sheria ifikapo Julai, mwaka huu. Tunamshauri kulingana na mazuri aliyoyaanzisha ndani ya jeshi letu, wako baadhi ya maofisa wake watamharibia kama ambavyo imeanza kujitokeza katika upandishaji huu wa sasa wa vyeo. Tunamuomba asidanganywe kuongezwa muda, ni vyema akastaafu ili heshima yake iendelee kuishi,” anasema askari mmoja kati ya wengi waliozungumza na Raia Mwema kuhusiana na taarifa hizi.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako